
Utangulizi
Dunia nzima kwa kipindi cha tangu mwishoni mwa mwaka 2019 mpaka sasa April 2020 imeingia katika mashaka makubwa kwa sababu ya mlipuko wa maambukizi ya ugonjwa wa Covid – 19 unaosababishwa na aina ya Virusi vya Corona. Zaidi ya watu Milioni 2 duniani kote wameambukizwa na ya watu 134,354 wamefariki huku watu takribani 511,356 wamepona. Idadi hii ni kwa mujibu wa taarifa kwa siku ya 15/04/2020. Bado imekuwa changamoto kubwa sana kwa dunia ambapo kila sekta imeathiriwa kwa sehemu kubwa. Hali ya kiroho, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na afya za wanadamu zimebadilika sana. leo tarehe 16/04/2020 ni takribani mwezi mmoja tangu maambikizi yameingia nchini kwetu Tanzania. Kasi ya maambukizi inaendelea kila siku na hofu kuu imetanda dunia yote, hakuna wa kumsaidia mwenzake. hii inaonesha ya kuwa hakuna taifa ambalo halijaathiriwa na janga hili iwe kwa maambukizi au kwa namna nyingine yoyote katika uchumi.
Kumekuwa na wito kutoka kila mahali namna bora za kujiepusha na maambukizi, huku wanasayansi wakikesha kutafuta SULUHISHO la janga hili ambalo limeikumba dunia yetu. Wito pia umetolewa kwa viongozi wa dini na waumini wa madhehebu mbalimbali kuendeleza sala na dua na maombi kwa Mungu ili aingilie kati kutunusuru na janga hili na kutuepusha sisi sote.
Kwa taaluma yangu mimi si mtaalam wa masuala ya afya hivyo napenda kusisitiza kwa wasomaji wote kuendelea kuzingatia kwa umakini maelekezo yanayotolewa na mamlaka ya Afya katika Taifa letu. Hatahivyo, nikiwa kama mwananchi wa kawaida wa Taifa langu Tanzania na mwamini katika Yesu Kristo ningependa kutumika kutoa mchango wangu wa mawazo katika upande wa KIROHO ili kuendeleza juhudi ambazo zinachagizwa na viongozi wetu wa kidini au kisiasa hasa katika kuliombea Taifa letu na dunia yote kwa ujumla tuepukane na janga hili.
Nitoe angalizo mapema juu ya makala hizi zina malengo kadhaa;
- Kuhamasisha Kanisa kuingia katika maombi maalum kwa lengo la kupata msaada wa Mungu katika kipindi hiki
- Kuendelea kusisitiza juu ya kuzingatia miongozo ya kiafya tunayopatiwa na wataalam wa Afya au Viongozi wahusika
- Kuendelea kupeana moyo na matumaini ya kuwa hatimaye tutavuka na kuona mwanzo mpya.
Makala hizi na uchambuzi wake utazingatia ufafanuzi tunaoupata katika maandiko matakatifu yaani BIBLIA. Hivyo ninapenda kukuhamasisha na wewe msomaji kupata muda wa kupitia maandiko haya kwani kwa ufahamu wangu tunaweza kupata majibu na kuchukua hatua zinazostahili ili kuliponya taifa letu.
Mataifa mengi yalifanya siku ya maombi ya tarehe 23 Machi 2020 kuhusiana na janga hili la Corona na wengi walitumia maandiko ambayo ningependa kuyanukuu pia;
‘Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao’ 2.Nyak.7:13 – 14
Haya ndiyo maneno ambayo viongozi wetu wameendelea kutukumbusha bila kujali nafasi zao kwamba tunamuhitaji Mungu wakati kama huu.
Katika mfululizo wa makala hizi na maombi tutamwomba Mungu atujalie neema yake ya kuyafahamu maandiko ili tuweze kuyaweka kwenye matendo na kupata uponyaji ulioahidiwa katika maandiko haya.
Nakukaribisha sana mtu wa Mungu ambaye utapata neema kushirikiana nasi katika safari hii kumtafuta Mungu aliyeziumba mbingu na nchi, aliye mfalme wa dunia yote mwenye kujua hatma yetu sisi wa kizazi hiki ili tukazione nguvu zake na msaada wake wakati huu tunaopitia.
Nikutie moyo ndugu yangu ya kuwa huu si wakati wa KUKATA TAMAA kama watu wasio na Mungu bali ni wakati wa kuongeza imani yetu kwa Mungu na kukuza uhusiano wetu pamoja naye. Hii ni safari ya kizazi chetu kushuhudia upande wa Mungu ambao hatujawahi kuushuhudia. Sisi nasi tunaweza kuingia katika historia ya vizazi vijavyo ya kuwa walikuwepo watu katika Kanisa la Mungu miaka ya 2020 ambao walisimama na Mungu wao. Mtu huyo ni WEWE na MIMI.

Karibu sana, tuendelee kuombeana katika kutimiza wajibu huu mkubwa tuliopewa kwa ajili yetu, nyumba zetu, taifa letu na ulimwengu mzima. Roho Mtakatifu atupake mafuta ya roho ya neema na kuomba ili kuyatimiza makusudi yake.
Maombi ya leo
Ee, Mungu Baba uliyeziumba mbingu na nchi na vyote ndani yake, unayejua majira na nyakati za maisha ya wanadamu kizazi na kizazi, tunakushukuru kwa neema yako ya uhai uliyotupatia. Tunaomba utujalie moyo wa unyenyekevu ili tuweze kukujia wewe kwa njia ya maombi, sala, dua na shukrani. Ninakuomba unijalie mimi………………………………………………… kuwa sehemu ya kutafuta suluhisho ya janga hili kubwa linaloikumba dunia yote, nikafanyike baraka kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, Taifa langu na hata dunia yote kwa kazi ambazo nitafanya kwa utukufu wa Jina lako na mwana wako Yesu Kristo. Amen
# Sauti ya Matumaini # Toba ya Dunia
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Ameen Ubarikiwe sanaa Mtumishi.
Asante ubarikiwe sana
Amen brother