
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tulijifunza juu ya kusudi la chakula. Leo tunaendelea kuona zaidi juu ya kusudi la chakula.
‘Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula’ 2.Theth.3:10
Haya ni maneno ya Mtume Paulo akiwaagiza kanisa la Wathethalonike juu ya umuhimu wa watu wote kuwa na kazi ya kufanya. Tumezoea msemo huu mara nyingi unaosema ‘ asiyefanya kazi na asile’. Kupitia andiko hili tunaweza kujifunza zaidi juu ya makusudi ya chakula kwa maisha ya mwanadamu. Makala iliyopita tuliona kusudi kuu la chakula ni kuhifadhi uhai yaani tunakula tuweze kuishi, leo tunajifunza kusudi lingine la kwa nini tunakula chakula.
Mambo ya kujifunza
• Tumesikia mara nyingi juu ya neno ya kwamba ‘asiyefanya kazi na asile’. Hii ina maana kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya kazi na chakula.
• Kwa tafsiri inayoonekana wazi ni kwamba chakula ni matokeo ya kazi ya mtu. Yaani ili mtu ale ni lazima afanye kazi ya kumletea kipato cha kumwezesha kula.
• Hatahivyo kwenye neno hili unaweza kuona tafsiri nyingine inayosema ‘tunakula ili tuweze kufanya kazi’ yaani chakula ni nyenzo ya kutuwezesha kufanya kazi.
• Sote tunaweza kuona ukweli huu katika maisha ya kila siku ya utendaji wa kazi wa miili yetu. Ufanisi wetu katika kazi ni matokeo ya chakula tulichokula kukatupa nguvu ya kutimizi majukumu yetu ya siku kwa siku.
• Kama tunakubaliana uhusiano uliopo kati ya chakula na kazi. Basi kazi zetu za kila siku ni matokeo ya chakula tunachokula.
• Je, ni kitu gani tunalisha kila siku kati ya roho, nafsi na mwili? Majibu ya swali hili kila mtu anayo ya kwamba miili yetu ndio tunaipa kipaombele na inatulazimisha kuamka kila siku kwa lengo la kuishibisha. Tuna mpango madhubuti kabisa wa chakula kuhusu miili yetu. Hatuna nafasi juu ya roho wala nafsi zetu.
• Kama roho na nafsi zetu hazipo kwenye mpango wa chakula kila siku ni dhahiri hatuwezi kuona kazi za kiroho kwenye maisha yetu. Wengi wetu tunakwenda kuudhuria ibada siku ya Jumapili. Wiki nzima hatujapata nafasi ya kulisha roho zetu na nafsi kwa neno la Mungu hata kwa kujisomea wenyewe. Je, tunaweza kuwa hai kama hatujala chakula cha mwili kwa siku 6? Je, tunaweza kufanya kazi zetu kama kawaida endapo hatujapata chakula cha mwili kwa siku 6? Jibu ni hapana. Kwa nini tunafikiri hali yetu ya kiroho haitoathiriwa hata kama hatujapata chakula cha kiroho kwa siku 6?
• Hatupaswi kuishia kulisha miili yetu tu, ni lazima tuwe na mpango wa namna ya kulisha nafsi zetu na roho zetu kwa chakula cha kiroho kila siku kwa lengo la kuweza kuziwezesha ziingie kazini.
• Chakula cha kiroho ni nyenzo ya kumwezesha mwanadamu kutenda kazi za Mungu hapa duniani. Hatuwezi kutimiza makusudi ya Mungu kwa kutegemea chakula cha kimwili. Ni lazima tujue na tutafute kupata kila siku chakula cha kiroho kama tunataka kuyatenda mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Nazid kupata vitu hapo ni muhimu Sana kweli tujitafakari na ndio maana Kuna baadhi ya Mambo mabaya yanatokea ktk maisha yetu kumbe sababu kubwa pia ni kutompa Mungu kipaombele tumetanguliza Mambo yetu mengi kuliko kumtanguliza Mungu, na lait tungeweza kwa sehem kidogo Kama baadhi ya waislam wanaothamin Ibada nazan Wakristo tungekua mbali Sana ila changamoto yetu kubwa NEEMA tuliyonayo ndio inatufanya tuone kila kitu ni sawa tu na kuona siku ya Ibada ni jumapil tu! Kumbe sivyo Ibada ni kila siku …. Mungu atuponye katika hili…
Asante kwa somo zuri… God bless you.. ???
Karibu sana Victor ni kweli suala la roho zetu na nafsi zetu zinapaswa kupewa kipaombele cha kwanza ili kufanikisha mambo mengine yote. Bwana Yesu alisema utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake na hayo mengine mtazidishiwa. Hali yetu ya kupungukiwa na hayo mengine mengi ni kutokana na kupoteza focus ya maisha. Karibu sana na endelea kusambaza ujumbe huu kwa wengine wengi wapate maarifa haya.