
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wa isaackzake. Pia nikukaribishe katika ukurasa huu maalum kabisa kwa lengo la kufuatilia mambo mbalimbali tunayotarajia kujifunza kwa lengo la kuboresha maisha yetu. Moja ya eneo ambalo linaathiri maisha yetu kwa sehemu kubwa ni aina au mfumo wa elimu ambao tumepitia. Mfumo huo unaweza kuwa rasmi au usio rasmi, kwa vyovyote vile aina ya elimu ina sehemu kubwa sana katika kuamua hatma ya maisha yetu. Katika makala ya utangulizi tumeutambulisha Mfumo Mbadala wa Elimu. Leo tunataka kujifunza zaidi juu ya ‘Maana ya Elimu’ Karibu
Tafsiri ya Elimu
Watu wengi tumeenda shule na kuhitimu ngazi mbalimbali za mafunzo lakini ukiuliza kwa hakika juu ya tafsiri ya neno elimu si wengi wanaweza kukupa majibu ya moja kwa moja. Mtu anaweza kusema elimu ni ngazi ya vidato au shule alizosoma, mwengine anaweza kusema ni ujuzi aliopata. Mtazamo wa kijamii kwa sehemu kubwa unahusisha suala la elimu na kuudhuria katika madarasa au vyuo. Tunadhani ya kuwa wale waliopata nafasi ya kwenda darasani na kufikia ngazi za juu basi ndio jamii ya walioelimika huku wengine tukiona hawana elimu.
Tuangalie kwa sehemu tafsiri ya neno elimu na jinsi linavyoweza kutumika kuhusisha kila mmoja wetu bila kujali ngazi ya vidato au madarasa tuliyopitia au ambayo hatujafikia.
Neno ‘elimu’ ambalo kwa lugha ya kiingereza linatafsiriwa kama ‘education’ lina maana pana sana zaidi ya kitendo cha mtu au watu kwenda kwenye maeneo maalum ya kujifunza yaani shule au vyuo. Neno ‘education’ linatokana na neno la kilatini ‘educo’lenye maana ya ‘kuongezeka/kukua kutoka ndani au kukua kiakili au kuwa na nguvu’ au ‘to develop from within, to grow in mind, to have power’.
Hivyo kwa tafsiri pana zaidi neno elimu linaweza kusemwa kama ‘ni kitendo au mchakato wa kupata jumla ya maarifa, kukua kwa uwezo wa kufikiri au kuamua na kujiandaa binafsi kimaisha’ (tafsiri hii kutoka kwenye kitabu cha The Business World & What School Didn’t Teach You About Business na Titus Mirieri, uk.7)
Ukiitazama tafsiri hii kwa mapana yake unaona dhahiri suala la elimu si lazima kwa watu kuhusika na kuingia katika madarasa ingawa eneo la madarasa au shule au chuo ni mojawapo ya maeneo ambapo elimu huweza kupatikana. Upana wa tafsiri hii unahusisha pia maeneo au vyanzo vingine nje ya mfumo rasmi wa elimu kuwa sehemu ya kumwandaa mtu kiakili katika safari ya maisha.
Maisha yetu kwa sasa yameathiriwa kwa sehemu kubwa sana na tafsiri tuliyonayo juu ya neno ‘elimu’ ikiwa tuliambiwa au kuaminishwa maana ya neno hilo basi ndio matokeo tuliyonayo.
Tafsiri sahihi ya neno au dhana yoyote katika maisha ndio msingi wa kupiga hatua na kujikomboa kifikra na kuondoa ujinga.
Elimu ni kitendo au mchakato wa kupata maarifa unayohitaji kwa ajili ya kujiandaa na kuishi maisha yako binafsi. Hivyo si wote walioenda darasani hata ngazi za vyuo wameelimika na si wote ambao hawakupata nafasi ya kuingia darasani ni wajinga. Muhimu kila mmoja na nafasi yake aliweza vipi kujipatia maarifa ya kuweza kumudu changamoto za maisha yake.
Hii ndio tafsiri ya neno ‘elimu’ ambayo tutaendelea kujifunza hatua kwa hatua. Endelea kufuatilia ukurasa huu wa ‘Mfumo wa Elimu Mbadala’ tunapoendelea kuzichambua dhana mbalimbali.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!