
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wa mtandao wa isaack zake hasa katika mfululizo makala maalum zinazohusu familia. Kama tunavyofahamu familia au muungano wa mtu mke na mtu mume ndio asili au chanzo cha uwepo wa jamii nzima na mataifa yote duniani. Leo hii tunazungumzia wakaazi wa dunia takribani Bilioni 7.8 wote hawa wametoka kwenye familia.
Makala iliyopita ya utangulizi ilianisha au ilichagiza fikra zetu hasa katika kuona changamoto tulizonazo jamii yote ya dunia kwa sasa katika muundo wa familia, namna zinavyoanzishwa na hasa namna zinavyoendeshwa. Matatizo mengi hapa duniani ni matokeo ya chombo hiki cha familia kutokuwa katika mwelekeo sahihi.
Leo tunataka kuangalia ni nini hasa chanzo cha madhila yote haya ambayo yanaikumba dunia. Karibu tujifunze.
Mwanadamu ni kiumbe anayeendesha maisha yake yote kwa kutegemea taarifa ‘information’. Jinsi mimi nilivyo au wewe msomaji ulivyo sasa ni matokeo ya jumla ya taarifa ambazo nimezipokea/umezipokea tangu kuzaliwa kwangu hata sasa. Tunaweza tusielewe ukweli huu au tusikubali lakini ndivyo ilivyo. Unaweza kuchunguza mwenyewe kuhusiana na vitu unavyopenda, mtu uliyeanzisha naye mahusiano, mahali unapofanya shughuli zako, aina ya shughuli unazofanya, nk vyote hivyo vimetokana na aina ya taarifa ulizosikia na ukachukua maamuzi yako binafsi.
Suala la kuunda na kuendesha familia halikadhalika tunalifanya kutokana na taarifa tunazopokea katika vyanzo mbalimbali. Wengine wanaanzisha familia kutokana na misingi waliyofunzwa na wazazi wao, kutokana na mambo wanayofanya wenye rika lao, kutokana na wanachojifunza katika mifumo ya elimu n.k
Jambo muhimu ambayo tunapaswa kujiuliza ni aina gani ya taarifa tulizopokea ambazo zinabeba tafsiri ya familia katika akili zetu? Ni nini kusudi la familia tunalobeba ndani yetu? Kwangu familia ina maana gani na ipo kutimiza kusudi gani?
Mfumo wa maisha yetu unawasukuma watu wengi ya kuwa baada ya kuzaliwa anajifunza, kisha anapata shughuli na hatimaye anaanzisha familia na kupata watoto kisha kuwapeleka shule nao baadae wapate kazi na kuanzisha familia. Hivi ndivyo wengi wetu tumejenga mtazamo wa kifamilia.
Lakini, ni kweli ndivyo inavyopaswa kuwa? Yaani familia ni kuzaa na kulea watoto kisha wakue wapate kazi na wao kuanzisha familia zao?
Kuna msemo unaosema ‘where purpose is not known abuse is inevitable’ kwa tafsiri ya kawaida ni kwamba ‘pale kusudi lisipojulikana basi matumizi mabaya ya kitu hayaepukiki’. Hii ina maana kama mtu hujajua ni nini hasa kusudi la kitu ulichonacho basi huwezi kukitumia vizuri kwa ufanisi. Kushindwa huko kukitumia kunapelekea kutokea madhara makubwa zaidi kwa mtumiaji na hasa kitu chenyewe kukosa maana.
Hali kadhalika kwa suala zima la familia au ndoa kama watu tupo kwenye familia au ndoa lakini hatujajua ‘kusudi’ la uwepo wake matokeo yake ni matumizi mabaya yenye madhara kwenye maisha yetu na kupoteza kabisa maana ya uwepo wake.
Tunayo kila sababu ya kujiuliza maswali muhimu sana kwenye maisha yetu hasa ya kifamilia ili tuweze kutambua safari tunayopaswa kuwa nayo.
Maswali ya kutafakari
- Kwa nini nimeoa/kuolewa au kwa nini nimeanzisha familia?
- Kwa nini ninatarajia kuoa/kuolewa au kuanzisha familia?
- Ni aina gani ya familia au ndoa ninayotaka kuwa nayo?
Tafakari maswali haya kisha pata sehemu ya kitabu/daftari yako andika majibu hayo. Tutaendelea kujifunza zaidi katika eneo hili na kila mmoja aweze kutazama majibu yake ili kujua hasa kama tunayo tafsiri sahihi au la.
Wako
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Asante sana wakili kwa makala hii.Umezungumzia mambo yamsingi sana juu ya kuanzisha familia.
Wengi wanaendeleza familia kimazoea waliyoyakuta ndiyo wanayaendeleza na ndiyo maana changamoto hazikomi kizazi baada ya kizazi maana hatujui kusudi la familia tunazoanzisha ila tunafuata mkumbo,kwamba watu wa rika langu wameoa au kuolewa na mimi nafanya kama wao.
Karibu sana Hendry tuendelee kujifunza zaidi.