1. Familia

Utangulizi
Karne ya 21 ni wakati ambao mabadiliko makubwa katika mifumo ya maisha ya wakaazi wa dunia hii yametokea kwa kasi zaidi. Tunashuhudia mabadiliko katika maeneo mengi sana ya kimaisha. Tunaona jinsi sayansi na teknolojia ilivyochukua nafasi kubwa ya maisha yetu ya kila siku.
Mifumo ya maisha hasa namna ambavyo familia zinaanzishwa, zinalelewe na kukabiliana na maisha ya kila siku imebadilika kwa kiasi kikubwa sana. Hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na dunia yetu kuwa kijiji kwa sababu ya teknolojia.
Sisi ambao tumezaliwa mwishoni mwa karne ya 20 na tumeanzisha familia karne ya 21, tulizoea kusikia masimulizi ya wazazi wetu wa karne ya 20 jinsi misingi ya ndoa na familia ilivyokuwa zamani, jinsi ndugu walivyoishi kwa ushirikiano na upendo mkubwa.
Lakini sasa wakati wetu wa kuwa wazazi umefika, na tunaona changamoto mpya ambazo kizazi kilichopita hakikushuhudia hizo. Mfano nyakati zao wazazi walikuwa na muda wa kutosha kulea watoto endapo mzazi mmoja alikuwa akifanya kazi na mwengine kuangalia watoto. Hatahivyo, nyakati hizi kila mzazi anahangaika kufanya kazi na watoto wetu wamebaki kuangaliwa na wasaidizi au waalimu mashuleni.
Karne ya 20 kwa sehemu kubwa mifumo ya maisha kwa maana maadili na nidhamu vilitegemea ni nini hasa wazazi wanafunza watoto wao, lakini sasa kwa mwingiliano wa sayansi na teknolojia watoto wetu wanajifunza zaidi kupitia TV, mitandao ya kijamii, wapo you tube, instagram, tiktok n.k tamaduni zinaweza kutoka mbali sana lakini zikawafikia watoto wako chumbani kwao bila ya mzazi kufahamu kile kinachoendelea.
Kama wazazi tunaweza kuangaika sana na kufikiri ya kuwa elimu pekee ya darasani inaweza kuwavusha watoto wetu, lakini tunashuhudia namna ambavyo bado elimu haijaleta matunda kwa vijana wetu. Wanasoma, wanafaulu lakini wanaishia mtaani na kujiingiza katika tabia zisizofaa.
Changamoto haijaishia tu katika namna ya malezi bali hasa namna ya kuanzisha familia na uwepo wa ndoa. Miaka ya 1990 na huko nyuma zaidi ni nadra sana kusikia watu wametalikiana au kuona watoto wakilelewa na mzazi mmoja huku mwengine akiendelea na maisha yake. Lakini sasa talaka na malezi ya mzazi mmoja ‘single parenting’ yamekua sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kuna wimbi kubwa la wanandoa wengi kutalikiana au kuachana kuliko wale wanaoungana kuanzisha na kujenga familia.
Ukatili mkubwa tumeushuhudia nyakati hizi, habari za wanandoa kuuana au kuumizana, habari za mzazi kuwa na mahusiano ya kingono na mtoto wake, habari za watoto kudhulumiwa utu wao kwa kunyanyaswa na kudhalilishwa hasa na wanafamilia ni mambo ya kawaida kwa sasa bila kujali jinsia za watoto.
Tunazidi kuona changamoto kubwa ya vijana wetu au wale ambao taifa linawategemea kuanzisha familia hawana tena utayari wa kufanya hivyo. Tunaona ni mtindo wa maisha kwa vijana wa kiume kuzaa na kila mwanamke lakini hawana utayari wa kuanzisha familia na kuchukua majukumu. Mfumo umebadilika sana kiasi kwamba wanawake na mabinti kwa sasa wanahangaika kutafuta watu wa kuwaoa si kwa ajili ya kusaidiwa maisha lakini wanahitaji mtu wa kumwita mume, kiongozi wa familia.
Wimbi kubwa la watoto wanaoitwa wa ‘mitaani’ linazidi kuongezeka. Awali watoto hawa walijulikana kama watoto yatima, lakini kwa utafiti wangu mdogo nimeona watoto hawa wanatoka katika familia ambazo wazazi wao wote wapo hai lakini kuna shida ndani ya familia zinazowafanya waamue kuondoka nyumbani na kuanza kuishi ‘mitaani’ unakuta baba hayupo, mama na mtu mwengine na mahitaji ya mtoto hayatimizwi, hakuna wa kumfundisha nidhamu hivyo ni rahisi kuchukuliwa na makundi ya watu wengine.
Mtindo mpya wa maisha ambao unaenea sana sasa kwa vijana ambao una hatari kubwa zaidi ya mihadarati yaani maisha ya ‘kubet’ ni janga kwa mataifa ya Afrika. Tunashukuru sana kwa jitihada kubwa zinazofanywa na vyombo vya Serikali katika udhibiti mkubwa wa madawa ya kulevya, pombe kali, matumizi mabaya ya madawa n.k lakini sasa janga kubwa zaidi ni mtindo wa maisha ya kubashiri ‘kubet’ unakwenda kuhatarisha zaidi kizazi kijacho. Kama tunaruhusu vijana wetu kuingia katika mfumo huu wa maisha ni dhahiri imani ya kufanya kazi haitakuwepo na watabaki na mifumo ya kuishi kwa kubahatisha kila siku.
- Je, katika hali yote hii tunatarajia ni aina gani ya taifa la Tanzania tulaloliandaa kwa miaka 50 hadi 100 ijayo?
- Je, sisi wazazi wa nyakati hizi tumekuwa mfano bora kwa watoto wetu na vijana tunaowatunza kwetu?
- Je, Tanzania tuliyoikuta miaka 60 iliyopita baada ya uhuru ndiyo tunawarithisha vizazi vyetu ikiwa huru au inarudi katika ukoloni mbaya zaidi wa kifikra?
- Je, tukiondoka katika Tanzania sasa yaani maisha yetu yakifika ukomo, tuna uhakika wa mwendelezo mzuri wa familia zetu na taifa kwa ujumla?
Yapo maswali mengi sana kama mwanajamii najiuliza, pia naamini na wewe unaweza kujiuliza. Ni imani yangu kwamba endapo kila mmoja wetu ataishi misingi sahihi katika familia yake basi ni dhahiri taifa letu litapona na litavuka katika changamoto ambazo zinatukabili sisi nchi za Ulimwengu wa 3.
Viongozi wetu iwe wa kisiasa, kiroho, kijamii, wafanyabiashara, wazalishaji wote, na kila mmoja wetu ni zao la familia au ndoa. Sote tumetokana na familia au muunganiko wa mtu mume na mtu mke. Hivyo jinsi tulivyo kwa sehemu kubwa tumeathiriwa na mahusiano yao iwe kwa chanya au hasi. Kama jamii ina changamoto hizi zote, basi mzizi wake wa tatizo upo kwenye ndoa na familia. Kama familia zetu na ndoa zetu zitaimarishwa kwa maarifa sahihi ni wazi taifa letu na bara letu litakombolewa. Maana ndani ya familia ndio anatoka Rais, anatoka Jaji, anatoka Daktari, anatoka mfanya biashara, anatoka mwanamuziki, anatoka mkulima, anatoka Shehe au Mchungaji, anatoka mwalimu, anatoka askari au mhasibu nk. Maadili au utendaji wa hawa wote unategemea mazingira ya makuzi yao ndani ya familia.
Swali muhimu kwako na kwangu wazazi wa kipindi hiki tunawandaaje watoto wetu kwa miaka ijayo kwenye nafasi hizo?
Huu ndio msingi wa kuanzisha makala hizi za Familia, ili kwa pamoja tuzijadili changamoto zetu katika karne hii ya 21 na tuone hekima ya Muumba wetu ikituvusha salama.
Usiache kufuatilia zaidi makala hizi.
Wako
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.

Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!